Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachoongoza Halmashauri ya Jiji la Mbeya, jana kilisusia kikao cha kujitambusha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla wakimlalamikia kuvunja taratibu za protokali ya uongozi na kufanya kazi kwa misingi ya siasa.

Meya wa Jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi aliyekuwa kwenye ukumbi wa tukio awali, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha Mkuu huyo wa Mkoa kumpuuza kwa kufanya ziara kwenye Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa wakati ndiye ambaye anasilisimamia jiji hilo.

Mchungaji Mwashilindi alisema hayo alipopewa nafasi ya kuzungumza mwanzoni katika kikao hicho cha kumkaribisha Makalla mkoani humo, kilichohudhuriwa pia na baraza la madiwani pamoja na viongozi wengine wa dini na Serikali.

“Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu,” alisema Mchungaji Mwashilindi.

Baada ya tamko hilo, aliondoka ukumbini humo akifuatiwa na madiwani wake 34 wa Chadema.

Hata hivyo, Makalla alieleza baadae kuwa ameshangazwa na kitendo kilichoafanywa na Meya huyo kwakuwa alipokuwa ametembelea Shule ya Sekondari ya Iyunga alisema katika shule hiyo kuwa angetembelea soko la Mwanjelwa jana kabla ya kuingia kwenye kikao hicho.

“Mimi sijaja kufanya siasa nimekuja kufanya kazi ya wananchi na nilishatahadharisha jambo hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo siasa na wananilazimisha kufanya siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na wananchi. Na ninasema kama Mola ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa mwaka 2020 nitakwenda kuwaambia hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi wao,” alisema Makalla.

 

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi lapinga Panga la Magufuli kwenye Mishahara
Yanga waong’olewa na Al Ahly kwa ‘mbinde’