Mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika jana katika wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ulivurugika baada ya Jeshi la Polisi kuwatawanya wafuasi wa chama hicho kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.

Chadema walikuwa wamepanga kuzindua kile walichokiita ‘Operesheni okoa demokrasia nchini’, wakilenga katika kuishtaki Serikali kwa wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara katika mikoa mingine nchini.

Wakati polisi wakifyatua mabomu ya machozi na maji ya washawasha, baadhi ya wafuasi wa Chadema waliwarushia mawe kitendo kilichozua vurugu kubwa zilizodumu kwa takribani saa moja kuanzia majira ya saa 9 alasiri.

Wanachama hao waliokuwa wamekusanyika katika viwanja vya CDT mjini Kahama walikuwa wakisubiri msafara wa viongozi wa chama hicho ukiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Leman a wengine.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kuzuiwa kwa mkutano huo, Mbowe alieleza kusikitishwa na kitendo cha kuzuiwa kwa mkutano wao.

“Hizi ni siasa za kibabe na kidikiteta ambazo Rais Magufuli ameanza kuzionesha kwa kuzuia Bunge lisionekane na sasa wanazuia mikutano ya hadhara ambayo ni haki yetu kikatiba,” Mbowe anakaririwa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mshinji alieleza kuwa awali walipewa kibali na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya mkutano huo akiitaja barua ya kibali ya Jeshi hilo ya Juni 6 iliyosainiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama (OCD), George Kyando kwa masharti ya kutofanya maandamano, kutoa kashfa na vurugu.

Alisema kuwa wakati wanajiandaa kwenda mkutanoni majira ya Saa 6 mchana, walipokea nyingine kutoka kwa Jeshi hilo ikieleza kuwa wamezuiwa kufanya mkutano huo kutokana na sababu za kiintelijensia.

 

Zitto Kabwe aingia Mikononi mwa Polisi
Video: TFF Yatoa Tamko Uchaguzi Yanga, Na Mambo Mengine Haya Matatu