Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kimebaini makosa 17 kwenye orodha ya wapiga kura katika kituo kimoja cha kupigia kura cha Azimio kilichoko jijini Arusha, ikiwa ni hatua za kwanza za kulikagua daftari la wapiga kura waliojiandikisha kwa mfumo wa BVR.

Chama hicho kimeeleza kuwa moja kati ya makosa waliyoyabaini ni pamoja na kuwepo watu wanaoonekana kuwa ni wazungu na wachina katika orodha ya daftari la wapiga kura walilopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi amesema kuwa makosa kama hayo yameendelea kubainika katika vituo vingine 63,523 vilivyoko nchi nzima.

Reginald Munisi

Reginald Munisi

Munisi alieleza kuwa kati ya makosa hayo waliyoyabaini awali wakiwa wanaendelea kulikagua daftari hilo la wapiga kura, wamebaini pia kuwa baadhi ya wapiga kura walijiandikisha kama wanawake huku sura zao zikionesha kuwa ni wanaume. Pia, baadhi ya watu wamejiandikisha kuwa wamezaliwa mwaka 1990 lakini sura zao zinaonesha kuwa wana umri mdogo zaidi.

Aliongeza kuwa wamebaini baadhi ya picha za wapiga kura zinaonesha kuwa zilipigwa wakiwa katika migahawa, kwenye pikipiki pamoja na majumba mbalimbali lakini picha hizo zina namba za wapiga kura.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa pamoja na mapungufu hayo waliyoyabaini katika hatua za kwanza, bado NEC imekataa ombi lao la kuukagua mfumo wa kielekitroniki utakaotumika kuhesabia kura wakidai kuwa hawawezi kuwaruhusu waingine ‘jikoni’.

“Tunataka NEC iwaruhusu wataalam wetu kuukagua mfumo wa kujumlishia kura, kama hawataruhusu basi sisi tutachagua kuhesabu kwa mikono,” alisema.

Akijibu malalamiko ya Chadema, mtaalam wa Teknolojia na Habari wa NEC, Alphonce Nyambita aliwataka Chadema kujifunza kuiamini Tume hiyo.

“Nadhani hakuna kitu cha kuogopa, kila mpiga kura atafika katika kituo cha kupigia kura akiwa na kitambulisho chake chenye picha. Kwa hiyo haina maana kusema kuwa NEC imepanga kuhujumu uchaguzi,” alisema.

 

 

Baada ya Kuadhibiwa, Mourinho Atoa Ya Moyoni
Klopp: Nimebaini Jambo Kikosini