Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa hawatazingatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan la kusitisha mikutano ya hadhara na kuwa subira.

Akizungumza jana kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kudai Katiba Mpya lililofanyika Tabata Dar es Salaam, Mbowe alisema mikutano ya hadhara ni haki yao kikatiba. Hivyo, aliwataka viongozi wa chama hicho kujiandaa wakati wowote kufanya mikutano hiyo pale watakapotangaziwa.

“Kwanza tuna amani, mikutano ya hadhara ni haki ya kikatiba, kisheria na ni wajibu wetu, ombi la Mama Samia kwamba tusubiri, tumpe muda hatuko tayari kumpa muda. Natoa agizo kwa viongozi wote wa chama nchi nzima, wajiandae mapema kwa ajili ya mikutano ya hadhara siku ambayo tutaitangaza,” Mbowe anakaririwa.

Mbowe alidai kuwa nusu ya wabunge ambao wako bungeni hivi sasa hawakuchaguliwa na wananchi, hivyo kuwaruhusu wao ndio wafanye mikutano ya hadhara katika maeneo yao na kuwanyima nafasi hiyo wanasiasa wengine sio sahihi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari baada ya kukamilisha siku 100 za uongozi wake, Rais Samia aliwataka Watanzania kuwa na subira kuhusu Katiba Mpya na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, ili kumpa muda kuimarisha uchumi wa Tanzania ambao umeathiriwa na janga la corona.

Barbara: Young Africans wajiandae kwa kipigo
Mahakama Kuu ilivyopiga ‘stop’ uchaguzi TFF, yawaita viongozi