Chadema iliitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu jana kujadili homa ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kikao hicho kilifanyika jana na kuhudhuriwa na wabunge waliopewa adhabu ya kutohudhuria vikao viwili vya bunge hadi vyote vilivyosalia kwa kosa la kufanya fujo bungeni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu ya mafuta na gesi kwa hati ya dharura.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, manaibu katibu wakuu wa chama hicho, John Mnyika (Tanzania Bara) na, Salum Mwalimu (Zanzibar), walisema kuwa chama hicho kimelazimika kuitisha kikao hicho kilicho nje ya ratiba ya vikao vya chama kutokana na kuwepo haja ya kujadili mambo ya msingi yanayokikabili chama hicho kutokana na uwepo wa joto la uchaguzi mkuu.

Salum Mwalimu alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar matukio ya ufyatuaji risasi yanayofanywa na jeshi la polisi katika maeneo ya uandikishaji wapiga kura linatia shaka kwa kuwa sababu zinazotolewa na serikali haziridhishi.
Salum aliongeza kuwa yapo matukio yasiyo ya kawaida yanayojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa mfumo wa BVR hasa katika vituo vilivyo katika ngome ya Chadema.

“Wale walioandishwa mwanzo kwenye wilaya za Mlele mkoani Katavi na Kilombero, Morogoro wameambiwa warudishe kadi walizopewa na waandikishwe upya. Hii siyo hali ya kawaida na hasa inafanywa katika majimbo ambayo ni ngome ya Chadema,” alisema.
Naye John Mnyika, alieleza kuwa kikao hicho kilijadili maandalizi ya jumla ya Uchaguzi Mkuu,kupokea taarifa za wagombea udiwani, ubunge na urais, taarifa ya majadilainao ya Ukawa kuhusu wabunge waliopewa adhabu bungeni pamoja na lile la miswada iliyopitishwa bungeni.

“Chama kinaungana na wabunge wa Ukawa kumtaka Rais asisaini miswada hiyo. Tunazo taarifa kuwa uharakishaji huu unafanywa ili kutimiza mashart tuliyopewa na mataifa ya nje ikiwa ni pamoja na vigezo vya kupata fedha za mfuko wa millenia,” alisema Mnyika.

Avril Aweka Wazi Ujauzito Wake
CCM: Hatutachagua Mgombea Kwa Shinikizo La Wapambe