Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemrushia lawama Rais John Magufuli kuwa uamuzi wake ndio chanzo cha tatizo la uhaba wa sukari linaloikumba nchi hivi sasa.

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Moshi Vijijini ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu alipozungumza na waandishi wa habari jana kuhusu sakata la suakari lililoshika kasi na kufunika masakata yote yaliyokuwa mbele ya vyombo vya habari nchini katika kipindi cha hivi karibuni.

Komu alisema kuwa Rais Magufuli alitoa zuio la utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nchi za nje mwezi Februari bila kufanya tathmini ya kutosha.

Aidha, Komu alidai kuwa agizo la Rais Magufuli kutaifisha sukari iliyofichwa na wafanyabishara ni kupora haki za watu na kuua mitaji yao.

“Hakuna sheria ambayo inaruhusu kwenda kukagua maghala ya wafanyabiashara na kugawa bidhaa bure, hii hali hata wawekezaji wataogopa kuja kuwekeza nchini kwa sababu wataona mazingira ya hapa nchini ni hatarishi,” Komu anakaririwa.

Aliongeza kuwa Kambi ya upinzani haiwatetei watu walioficha sukari, lakini kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na BBC, mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 590,000 lakini ni tani 300,000 pekee ndio uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani. Hivyo, aliitaka Serikali kuwaruhusu wafanyabiashara hao kuagiza sukari ili kukabiliana na uhaba uliopo.

Hivi karibuni kumekuwa na kilio cha mfumuko wa bei ya sukari nchini huku mikoa mingi ikipata kiasi kidogo cha Sukari.

Katika kulikabili hilo, Rais Magufuli ameagiza wafanyabiashara wote walioficha sukari kutaifishwa sukari hiyo na kuigawa. Pia, Rais Magufuli ameowaondoa hofu wananchi kuwa Serikali inafanya mpango wa kuagiza sukari nje ya nchi ili waiuze kwa bei nafuu kwa wananchi.

 

 

SERIKALI KUAGIZA TANI 70,000 ZA SUKARI
Lionel Messi Awaombea Njaa Real Madrid