Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimejibu kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ya kuwataka viongozi wa chama hicho aliodai walitoa maneno machafu dhidi ya viongozi wa dini kutubu.

Askofu Kakobe alitoa kauli hiyo katika ibada ya Jumapili kanisani kwake, ambapo alisema kuwa kuna baadhi ya viongozi waandamizi wa Chadema waliwatukana viongozi wa dini kupitia mitandao ya kijamii, hivyo wasipotubu chama chao kitatumbukia kwenye shimo refu.

Aidha, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya viongozi hao akiwemo Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amendika ujumbe akipinga kauli hiyo ya Kakobe.

“Kama kweli Kakobe ameongea maneno haya, anapasawa kupuuzwa, yeye ndiye ametumbukia kwenye shimo, aliwahi kusema umeme hautawaka pale Serikali ilipopitisha nguzo za umeme nje ya kanisa lake, huyu, aliwahi kusema Mrema atakuwa Rais Huyu, can we trust him anymore,”? Ameandika.

“Chadema hatuombi kupendelewa na kiongozi yeyote wa dini, sisi tunataka, utu, demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu, uhuru wa mawazo, uhuru wa vyombo vya habari, tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya. Kiongozi yeyote wa Dini asiyetaka haya, amepungukiwa na utukufu wa Mungu,” Msigwa ameongeza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rombo kupitia chama hicho, Joseph Selasini naye amedai kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla ndiye anayepaswa kumuomba msamaha Askofu huyo na kwamba yeye ndiye aliyewahi kumtukana.

“Wafuasi wa Chadema walichosema kitu kidogo kwamba walitarajia Rais apewe ushauri hali ilivyo nchini. Watu kupotezwa, kupigwa risasi, kuuawa, demokrasia na haki za binadamu, utawala bora, katiba nk”, amesema Selasini.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameandika kuwa, “ni sawa kuheshimu watumishi wa Mungu. Ni baraka zaidi watumishi wa Mungu kumheshimu Mungu kwa dhati, kwa maneno, matendo, tabia na misimamo yao juu ya haki/matendo mema. Utumishi haupimwi kwa idadi ya waumini wala nguo za kitumishi. Ndio maana imeandikwa tutawajua kwa matendo yenu”.

Wiki iliyopita baada ya Rais Magufuli kuzungumza na viongozi wa Dini Ikulu jijini Dar es salaam, baadhi ya viongozi wa Chadema walionesha kutoridhishwa na jinsi ambavyo viongozi wa dini walivyomshauri Rais Magufuli kwenye mkutano wao uliooneshwa moja kwa moja kupitia TBC1.

Mchungaji Msigwa aliandika, “unapata wapi ujasiri wa kudai mafungu ya kumi kanisani?, Ujasiri wa kukemea watu kuvaa nguo fupi? ulevi? wizi? uzinzi?usengenyaji , uongo? Nk, wakati unakaa kimya unapoona maiti kwenye viroba, watu kupotezwa kutekwa na kuteswa  na wengine kuuawa? Mr. Preacher-man tuambie!”

Tuchel afunguka kuhusu Neymar na Manchester United
Marekani yamtega Maduro kwa mabalozi wake, ‘aguse aone’