Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Temeke, kimeanza ‘tumbua jipu’ kwa mtindo wa aina yake baada ya kumtimua uanachama diwani wa Kata ya Kurasini, Matiti Togocho kwa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Temeke, Berdad Mwakyembe alisema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa Togocho alitumia vibaya madaraka yake kufoji hati na kujipatia kifisadi shilingi milioni 250.

Alisema kuwa Togocho alitumia wanasheria feki kuonesha amri ya kuvunja nyumba za wakazi wa eneo lake badala ya kutumia amri ya mahakama hivyo kusababisha wananchi kulala chini ya miti kwa udanyanyifu wake.

Mwakyembe alisema kuwa wamemvua uanachama Togocho kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya chama hicho inayotumika kuwaadhibu wabunge na madiwani wanapokiuka kanuni na taratibu za uongozi.

Hata hivyo, Togocha hakuonesha kupinga au kukubaliana na adhabu hiyo huku akidai kusubiri tamko la ngazi ya juu zaidi.

“Unajua aliyeongea ni Mwenyekiti wangu, hivyo siwezi kuropoka kitu hadi nisikilize kutoka kwa Boss wangu ambaye ni Mratibu wa Kanda,” Togocho anakaririwa.

Kwa mujibu wa taratibu na kanuni, diwani au mbunge akivuliwa uanachama hupoteza sifa za kuwa katika nafasi hiyo.

Imeelezwa kuwa taarifa za kufoji hati tayari zimefikishwa kwenye ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya hatua zaidi.

Zitto amshauri Magufuli mazito kuhusu Escrow, Muhongo atoa neno
Matonya na vijana wake wamlilia Magufuli