Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema) kimemuomba rais John Magufuli kuingilia kati chaguzi za wenyeviti wa Halmashauri na Meya kutokana na kile walichodai ukandamizwaji wa demokrasia unaolenga kuwapora wapinzani ushindi katika baadhi ya Halmashauri wanazoongoza kwa wingi wa madiwani.

Mkuu wa idara ya Habari na Mawasiliano ya Chama hicho, Tumaini Makene amesema kuwa rais Magufuli anapaswa kuingilia kati ili haki iweze kutendeka kwa kuwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hivi sasa ziko chini ya Ofisi ya rais.

Makene ameeleza kuwa kuna maagizo yanayotolewa na maafisa waandamizi wa serikali kwenda kwa wakurugenzi wa Halmashauri wakiwataka kuhakikisha CCM inashinda kwa gharama yoyote kwenye halmashuri ambazo wapinzani wanaongoza.

“Uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ni ushahidi na pia kucheleweshwa kwa mchakato wa uchaguzi katika manispaa ya Kinondoni na Ilala jijini Dar es Salaam, hadi sasa hatuna taarifa lini tutawachagua viongozi wetu,” alisema Makene.

Uchaguzi wa Meya wa Kinondoni na Ilala uliahirishwa baada ya kutokea sintofahamu kati ya madiwani wa Chadema na madiwani wa CCM kuhusu utaratibu wa kufanya uchaguzi na watu sahihi wanaopaswa kupiga kura.

 

TRA Yafafanua Kuhusu Watumishi Wake Kutangaza Mali Zao
Walichozungumza Rais Magufuli na Maalim Seif walipokutana Ikulu Jana