Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepanga kutoshiriki katika mchakato wa kura za maoni ya Katiba Mpya inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vicent Mashinji ameeleza msimamo huo wa chama chake jana jijini Dar es Salaam, alipoupokea ujumbe wa chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya vyama hivyo kuhusu Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.

Alisema kuwa Chadema hawatashiriki mchakato wa kura za maoni badala yake wataendelea kuipigania Rasimu ya Katiba Mpya iliyobeba maoni ya wananchi iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Alisema katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba iliondoa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye rasimu hiyo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Dk. Mashinji alieleza kuwa chama hicho kitaendelea kupigania Katiba Mpya inayotoa vipaumbele vitakavyotatua matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii ya Tanzania.

Chadema ni moja kati ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uliozaliwa kutokana na vuguvugu la kupinga Rasimu ya Katiba iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba huku wakiyataka Rasimu ya Katiba iliyobeba maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa na Jaji Warioba.

 

Naibu Spika azua tafrani kwa kumuita Mbunge ‘Bwege’, Mnyika atishia Kumfikisha Mahakamani
Zitto Kabwe atema Cheche Bungeni, aing'ang'ania Takukuru