Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kinatarajia kufungua kesi mahakamani ya kupinga utaratibu uliotumika kumvua ubunge aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida mashariki, Tundu Lissu ambaye yupo nje ya nchi kwaajili ya matibabu.

Hayo yamesemwa mkoani Njombe na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alipokuwa akizungumza na waaandishi wa habari baada ya kuwasili mkoani humo.

Amesema kuwa utaratibu huo umekiuka sheria kwa sehemu kubwa kwakuwa utenguzi huo umefanyika wakati mbunge huyo akiwa katika matibabu na kwamba kuhusu kujaza fomu za maadili na mali amesema asingeweza kujaza kwa kuwa hakuwa ndani ya nchi na asingeweza kusainiwa kwa mujibu wa sheria

Aidha, amezitaja agenda zitakazojadiliwa katika ziara hiyo ambayo ameambatana na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe katika kanda ya Nyasa ni pamoja uchaguzi wa serikali za mitaa, kuwashukuru viongozi na wanachama kwa kazi kubwa waliyofanya wakati Mbowe na viongozi wa Chadema wakiwa mahabusu kwa zaidi ya miezi minne pamoja na kutoa ufafanuzi wa sheria mpya ya vyama vya siasa ambayo imeonyesha kubadili kwa kiasi kikubwa utendaji wa vyama nchini.

Nao baadhi ya viongozi wa chadema mkoa wa Njombe akiwemo Rose Mayemba kiongozi wa Chadema na Alatanga Nyagawa ambaye ni katibu wa mkoa chama hicho wamesema kuwa wameanza kuandikisha wanachama katika daftari maalumu la A3 kuanzia ngazi ya chini na kwamba Watanzania wategemee chama hicho kupata ushindi mkubwa kwa kuwa kimejiimarisha katika utunzaji wa taarifa.

Katika ziara hiyo Mbowe amekagua ujenzi wa jengo la ofisi za chama hicho mkoani humo iliyopo katika mtaa wa Hagafilo ilyofikia asilimia 95 katika ujenzi wake.

 

Yondani kukabidhiwa mikoba ya Ajibu #TetesizaSoka
Real Madrid wathibitisha kifo cha kaka yake Zidane