Mvutano wa uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) unatajwa kuwa ni tishio kubwa kwa umoja wa vyama vya siasa wa Ukawa ambao chama hicho ni sehemu ya nguzo kuu, hali iliyoibua maoni tofauti kati ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari, amekiri kuwa mgogoro huo utaiathiri Ukawa ambayo Profesa Ibrahim Lipumba anayeupigania uenyekiti wa CUF alikuwa mmoja kati ya waasisi wake lakini aliutosa baadae akipinga uwepo wa Edward Lowassa.

“Spirit ya Ukawa ni umoja uliojitokeza baada ya kuaminiwa na Watanzania. Sasa hali hii inaathiri kwa kiasi fulani,” Alisema Profesa Safari.

Profesa Safari aliifananisha hali hiyo na kuwa na golikiba mzuri wa timu ya mpira wa miguu ambaye ni mlemavu wa miguu.

Akizungumzia barua ya Msajili wa vyama vya siasa iliyoeleza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF, Profesa Safari alisema kuwa msajili anajua ukweli kuwa ushauri wake hauwezi kuchukuliwa kama uamuzi wa mwisho kumrudisha Profesa Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho lakini aliamua tu ‘kuvuruga’.

Alisema kuwa ili kupata uamuzi wenye mamlaka kisheria juu ya mgogoro huo, Profesa Lipumba anapaswa kwenda Mahakamani na sio CUF.

Hata hivyo, Mbunge wa Tarime vijijini (Chadema), John Heche alitofautiana na mtazamo wa Profesa Safari kuhusu mgogoro huo wa CUF akidai kuwa Profesa Lipumba hawezi kuuyumbisha umoja huo.

“Ukawa haiwezi kuyumbishwa na Lipumba, Ukawa ilianzishwa na wabunge [wa bunge la katiba] na sio ushawishi wa Liumba,” alisema Heche.

Juzi, Profesa Lipumba aliingia kwa nguvu ndani ya ofisi za makao makuu ya CUF zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam baada ya wafuasi wake kuvunja mlango na kuwapiga walinzi waliokuwa zamu.

Lipumba ameendelea kueleza kuwa yeye ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho huku akipinga maamuzi ya kusimamishwa uanachama yaliyotolewa na Baraza Kuu la chama hicho akidai kikao kilichofikia maamuzi hayo hakikuwa halali.

Kufuatia tukio la kuvunja ofisi na kuingia ofisini kwa nguvu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui  alisema kuwa wamemuandikia Lipumba barua ya kumtaka ajitetee mbele ya Baraza Kuu la chama hicho kwanini asichukuliwe hatua kwani kitendo hicho ni kinyume cha katiba ya chama.

Hata hivyo, Lipumba amesema hajaipata barua hiyo na wala haitambui.

Video: Mechi Wabunge Simba, Yanga yachangia sh. Mil. 187 waathirika tetemeko la Kagera
Nape ajibu ‘ya Marekani’ kuhusu sheria ya mtandao, awataka wajinyoshee kidole