Hatimaye wabunge wa Chadema ambao ni moja kati ya wale walioshindilia msumari kwenye kashfa ya RICHMOND iliyopelekea Edward Lowassa kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu, wamemkaribisha kwa moyo safi mbunge huyo wa Monduli katika chama chao.

Kufuatia taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kuwa mbunge huyo wa Monduli amepanga kuihama CCM na kuhamia Chadema, wabunge mbalimbali wa Chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania Bara wametoa maoni yao kuhusu taarifa hizo.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alieleza kuwa chama hicho ni kama kanisa linalowapokea watu wote wasafi na wenye dhambi, wenye nia ya kufanya toba.

“Chadema ni kama kanisa, hakataliwi mtu, tunahubiri habari njema ya wokovu, ukija hapa unatubu unaendeea kufanya kazi,” alisema Mchungaji Msigwa.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alionesha kutambua nguvu kubwa ya Lowassa ndani ya CCM na kueleza kuwa hiyo inajidhihirisha baada ya kuona jinsi ambavyo viongozi wa chama hicho wengi wameamua kukihama wakipinga utaratibu uliotumika kuliondoa jina lake kwenye mchakato wa kugombea Urais.

“Namkaribisha Lowassa Chadema, huenda safari yake ya matumaini ikaishia huku, akwa mwanachama au hata kiongozi,” Lema anakaririwa.

Wabunge wengine walioonesha nia ya kumkaribisha vizuri Lowassa ni pamoja na Lucy Owenya, David Silinde, Suzan Lyimo, na Pauline Gekul.

Hata hivyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee hakupenda kutoa maoni yake moja kwa moja na kueleza kuwa atatoa maoni baada ya Lowassa kutua katika chama hicho huku akibainisha kuwa anatambua kila mtu ana haki ya kwenda chama chochote ili mradi awe na tija.

Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa ambaye anatajwa kuwa moja kati ya wawania nafasi ya kugombea kupitia umoja wa vyama vya vikuu vya upinzani, Ukawa, alizungumzia taarifa hizo.

“Niatazungumza pale mambo yatakapokuwa sawa, siwezi kuzumgumza sasa, subirini… sasa hivi mambo mengi yanazungumzwa kwenye mitandao.”

Askofu Gwajima Aikana Sauti Inayomtusi Kardinali Pengo
Van Gaal Alikuwa Na Nia Ya Kuipasua Bayern Munich.!