Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Mkoani Iringa kimesema kuwa kinakamilisha taratibu za kulishtaki Jeshi la Polisi, kwa kuvamia, kujeruhi na kuharibu mali katika hoteli inayotumika kama sehemu ya kambi ya kampeni ya chama hicho.

Jeshi la Polisi mkoani humo lilivamia katika hotel moja inayodaiwa kuwa kambi ya kampeni ya chama hicho na kuwakamata wafuasi 62 na baadae kumtafuta na kumkamata Mbunge wa Iringa Mjini anayetetea nafasi yake, Mchungaji Peter Msigwa kwa madai ya kula njama na kuwafanyia fujo wafuasi wa CCM waliokuwa wanatoka kwenye mkutano wa kampeni.

Akiongea na waandishi wa habari jana mjini humo, Mchungaji Msigwa ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Iringa Mjini,Frank Nyarusi, alilalamikia utaratibu uliotumiwa na jeshi la polisi kuvamia na kuwakamata wafuasi wa chama hicho siku tatu zilizopita.

“Kwa sababu tumejiridhisha pasipo mashaka yoyote, yaani without reasonable doubt, kwamba yuko hapa kwa ajili ya kukandamiza na kubaka demokrasia. Tumetoa taarifa kwa chama taifa na tumepata baraka zote kusoma press hii. Na wanasheria wetu chama Taifa wanaandaa namna gani waweze kulishitaki jeshi la polisi kwa jinsi lilivyofanya uharibu na kuonea pamoja na kukandamiza haki yetu ya kutenda kazi kwenye chama hiki, alisema Msigwa.

Awali, Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhani Mungi alisema kuwa jeshi hilo lililazimika kutumia nguvu kuwakamata wafuasi 62 wa Chadema Mkoani humo, kwa kosa la kuwafanyia fujo wafuasi wa CCM waliopita katika eneo lao la kambi ya kampeni.

 

 

Magufuli Awaeleza Ukweli Wana-Singida
Mzunguuko Wa Tano Ligi Kuu Kuendelea