Hatimaye Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana usiku kilimpitisha Dk. Vicent Machinji kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Chama hicho katika kikao kilichofanyika jijini Mwanza, akichukua nafasi iliyoachwa na Dk. Wilbroad Slaa.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alikamilisha zoezi lililokuwa linasubiriwa kwa hamu na viongozi pamoja na wafuasi wa chama hicho kwa kulipendekeza jina la Dk. Machinji, jina ambalo lilipitishwa moja kwa moja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Hata hivyo, Dk. Machinji hakuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuvaa viatu vya Dk. Slaa, lakini inaonesha kuwa alikuwa mchezaji mzuri ndani ya chama hicho ambaye hakuwa anamulikwa na ‘spotlight’ za vyombo vya habari.

Hii ni ‘CV’ ya Dk. Machinji:

Dk Mashinji aliyezaliwa katika Wilaya ya Sengerema, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 mpaka Oktoba 1991 alipohitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kuanzia Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita.

Dk. Vicent Machinji, Katibu Mkuu wa Chadema

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari. 

Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na mwaka 2007-2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).

Hivi sasa ni mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii anayosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria. 

Rais Magufuli ateua Wakuu wa Mikoa wapya, Makonda aikwaa Dar
Mbowe afunguka kuhusu 'Lowassa kutoa pesa ili Ajiunge Chadema'