Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema Mwenyekiti  wa Chadema Taifa, Mhe. Freeman Mbowe atashindwa kuhudhuria ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa marudio wa Ubunge katika jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma siku ya Jumapili kutokana na kesi iliyopo Mahakamani.

Mrema amebainisha hayo wakati alipokuwa Mahakama Kuu ilipotupiliwa mbali ombi la marejeo ya uendeshaji wa kesi yao ya kufanya mkusanyiko usiokuwa wa halali mnamo Februari 17 mwaka huu kwenye chaguzi ndogo za marudio Jimbo la Kinondoni Jijini Dar es Salaam huku wakipewa nafasi ya rufaa juu ya maamuzi hayo yaliyotolewa na Mahakama.

“Kiukweli hizi kesi zinazoendelea Mahakamani zinatuathiri sana sisi kama chama, maana hadi sasa hivi hatujui ni nani ambaye ataweza kuenda kuzindua kampeni za uchaguzi wa marudio katika jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma siku ya Jumapili kutokana na viongozi wote wapo jijini Dar es Salaam wanafuatilia kesi zao”, amesema Mrema.

Pamoja na hayo, Mrema ameendelea kwa kusema “kikawaida alipaswa aje Mwenyekiti wa chama Freeman Mbowe lakini kwa hali jinsi ilivyo hatoweza kushiriki na sasa tunamtegemea Naibu Katibu Mkuu bara John Mnyika aje mara moja kufanya ufunguzi na kurudi zake kusikiliza mwenendo wa kesi”.

Wanachadema wanaoshtakiwa ni pamoja na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara John Mnyika, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salim Mwalimu.

Wengine ni Mbunge wa Tarime vijijini John Heche, Mbunge Tarime mjini Esther Matiko, Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.

Wote hao wanaandamwa na mashtaka 13 ikiwemo la kufanya mkusanyiko isiyokuwa na kibali kwenye chaguzi ndogo za marudio Jimbo la Kinondoni Jijini Dar es Salaam zilizofanyika Februari 17, 2018.

Kalinic aigomea medali yake ya kombe la dunia
Video: Fatma Karume arusha kombora Lugola ajibu, CCM mambo moto moto