Chama  cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimewapitisha makada wake wawili, Ezekiel Wenje na Lawrence Masha kugombea nafasi za ujumbe katika Bunge la Afrika Mashariki katika uchaguzi utakaofanyika mapema mwezi ujao.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara, John Mnyika alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa makada hao wamepitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho mara baada ya kupitia sifa na vigezo vya makada kadhaa walioomba nafasi hizo.

Aidha, Mnyika, amesema kuwa CHADEMA ina nafasi mbili kati ya 9 za uwakilishi kwenye bunge hilo kutoka Tanzania, na wao wameamua kupitisha majina mawili pekee ili kurahisisha kazi wakati wa uchaguzi.

“Kulingana na uwiano wa wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CCM wana nafasi 6, CHADEMA tuna nafasi mbili, na CUF wana nafasi moja, kwa hiyo tumeamua kupitisha majina mawili pekee ambayo sasa yatasubiri baraka za wabunge wa Bunge la Tanzania,” amesema Mnyika.

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa makada waliopitishwa wamewahi kuwa mahasimu wakubwa wa kisiasa hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo wote wawili walikuwa wakigombea jimbo moja la Nyamagana Jijini Mwanza wakiwa vyama tofauti.

Wakati huo, Masha alikuwa CCM, na alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani huku akitaka kulitetea jimbo lake, lakini alijikuta akipata upinzani mkali kutoka kwa Wenje (CHADEMA), ambapo matokeo yalimuangusha Masha na Wenje kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano kabla ya kuangushwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 na Stanslaus Mabula (CCM)

Makontena 262 ya mchanga wa dhahabu yanaswa bandari ya Dar
Watumishi wa umma watakiwa kuchangamkia fursa