Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa hii leo amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Hafla hiyo, iliyofanyika hii leo Mei 26, 2023 katika ofisi za Mkuu wa mkoa wa Kagera zilizopo Bukoba Manispaa, ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya za Mkoa huo, ambapo Fatma Mwasa amewahimiza wakazi wa Mkoa huo kutumia vyema fursa zilizopo ili kuchochea maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akiwa ofisini kwake pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

Mwassa amesema “Mkoa wa Kagera sio masikini tuna misimu miwili ya mvua kwa mwaka lakini pia tuna uvuvi wa samaki na dagaa na pia kuna senene kwakweli sasa tunataka kuhamasisha vizuri ijulikane kwamba huu uzalishaji unatoka Kagera.”

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewasisitiza wananchi wa Mkoa wa Kagera kumpa ushirikiano Mkuu huyo mpya wa Mkoa huo na kumuomba kuendeleza miradi na kutatua migogoro ya wakulima na wawekezaji pamoja na changamoto za mipakani.

Baadhi ya viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Amesema “Najua wewe ni hodari wa kutatua migogoro huko ulikotoka na hapa kuna migogoro vile vile, ila hapa kuna Ranchi zinazomilikiwa na mashirika na kwenye Ranchi kule huwa kuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kati ya vijiji na Ranchi, kuna tume ambayo imeundwa na waziri Mkuu ambapo tunasubiria baada ya mda mfupi watakuja na mwafaka mzuri ili tuweze kumaliza mgogoro huo.”

Fatma Mwasa, amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kumhamisha kutoka mkoa wa Morogoro, huku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amehamishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mei 15, 2023.

Pensheni za Wastaafu zinalipwa kwa wakati - Katambi
Nicolas Wadada huyooo Singida Big Stars