Timu ya Acacia Stand United FC maarufu kama Chama la Wana imejizatiti vilivyo kuelekea mchezo wake wa kesho wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Maafande wa jeshi la kujenga taifa (JKT – Ruvu) kutoka Pwani.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Afisa habari wa “Chama la Wana’” Issac Edward amesema wako vizuri kuwaangamiza maafande hao na kuzoa pointi zote tatu ili kuwapa furaha mashabiki wao ambao waliikosa katika mchezo wao uliopita walipofungwa nyumbani dhidi ya Simba SC.

“Kwakweli tumejidhatiti vilivyo kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya JKT Ruvu,”alisema. “Tuna kila sababu ya kushinda mchezo huo licha ya kuwa maafande hao wana kikosi kizuri na benchi la ufundi lenye watu wazoefu na soka la Tanzania lakini haitakuwa sababu ya kushindwa kuwapa kichupa, ”alieleza Edward.

Afisa habari huyo alisema kuwa kikosi chao kinazidi  kuimarika kila kukicha na pia ujio wa wachezaji wao Haruna Chanongo na Abuu Ubwa kambini umeongeza Morali kambini.

“Hali ya kikosi hivi sasa iko vizuri na Morali kwa wachezaji ni ya juu sana ukizingatia Haruna Chanongo na Abuu Ubwa wamejumuika na kikosi kambini toka siku ya jumatatu na wameendelea na Programu za mwalimu kama kawaida.

“Hapana shaka panapo majaaliwa yake Mwenyezi Mungu na kutokana na mfumo wa mwalimu Patrick Liewing na mahitaji yake basi siku ya kesho watashuka dimbani kuisaidia timu,” anakaririwa.

Pia amewaomba mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo pendwa mkoani shinyanga kujitokeza kwa wingi kuishangilia kwani katika kipindi hiki cha mzunguko wa pili wa ligi,timu inahitaji sana kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwao ili ifanye vizuri katika michezo yake ijayo na hatimae kushika nafasi za juu pindi ligi itakapo fikia tamati.

“Wajitokeze kwa wingi siku ya kesho katika uwanja wa kambarage kuishangilia timu yao ili iweze kupata matokeo mazuri ya ushindi ili tuweze kukaa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi,”alisema.

Acacia Stand United Fc kesho inashuka dimbani katika uwanja wake wa nyumbani CCM Kambarage mjini shinyanga kucheza na JKT Ruvu ikiwa ni muendelezo wa michezo ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

 

Nape Nnauye Amtimua Katibu Mtendaji BMT
Jamal Malinzi Asambaza Ujumbe Wa Kupanga Matokeo