Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Simba Adam Kingwande amejiunga na Stand United ya mkoani Shinyanga akitokea Kagera Sugar kwa kandarasi ya mwaka mmoja.

Stand inayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji wa madini ya ACACIA imeanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuwasainisha wachezaji waliofanya vizuri katika ligi iliyomalizika. Mbali na Kingwande wachezaji wengine waliosajiliwa ni Erick Mlilo na Miraji Maka toka Toto African ya Mwanza.

Afisa Habari wa klabu hiyo Deo Kaji Makomba amesema kuwa usajili huo umezingatia matakwa ya kocha wao Mfaransa Patrick Liewig kwa kuziba sehemu zenye mapungufu  ndani ya kikosi hicho.

“Ripoti ya mwalimu ndiyo tunaifanyia kazi, tunaendelea kujipanga kwa ajili ya msimu ujao na bado tunawaangalia wachezaji wengine wa kuwaongeza,” alisema Makomba.

Adam Kingwande ( kushoto ) alipokua anaitumikia klabu ya African Lyon.

Wakati huo huo Stand maarufu kama ‘Chama la Wana’ wapo katika hatua za mwisho za kuingia mkataba na kocha msaidizi raia wa Ufaransa  Guillaume Denis ambaye atakuwa pamoja na Athumani Bilali kumsaidia Liewig.

“Mazungumzo yanaendelea vizuri muda si mrefu tutaingia nae kandarasi kwa ajili ya kuitumikia timu yetu msimu ujao,” alisema Makomba.

5 Kubwa kutoka Magazeti ya Leo
The Blues Wamhalalisha Michy Batshuayi