Jose Chameleone ameripotiwa kugeuka mbogo na kuwafukuza kwa panga baadhi ya waombolezaji waliofika nyumbani kwa marehemu Mowzey Radio, eneo la Makindye jijini Kampala.

Kwa mujibu wa gazeti la The Vision la Uganda ambalo limeweka picha ya tukio hilo inayomuonesha mwimbaji huyo akiwa na panga na baadhi yawaombolezaji wakitafuta namna ya kuokoa maisha yao, limeeleza kuwa vuguvugu hilo lilisababishwa na uwepo wa msanii ambaye marehemu aliacha maagizo asihudhuria msiba wake kutokana na ugomvi kati yao.

Imeelezwa kuwa Chameleone alipata maelekezo kutoka kwa mdogo wake, Weasel kuwa Radio aliwahi kuapa kwamba msanii Shafick Walukagga aka Fik Fameika hatakiwi kuonekana kwenye msiba wake.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Chameleone ambaye alikuwa ndani kwenye ghorofa ya kwanza, aliagiza walinzi waangalie kwa makini wasiruhusu msanii huyo kuingia.

Hata hivyo, walinzi walishindwa kumtambua na kwa bahati mbaya aliingia ndani na taarifa zikamfikia Chameleone.

Chameleone anadaiwa kuchukua panga na kuondoka haraka akimtafuta msanii huyo. “Leo nitamchinja, atoke nje ya nyumba hii,” Chameleone anadaiwa kusikika kabla hajaanza kumsaka mbaya wake.

Hata hivyo, watu wa karibu wa msanii huyo walifanikiwa kumtorosha na ndipo Chameleone akawageukia waombolezaji wengine waliokuwa upande huo na kutishia kuwakata panga, hivyo wakatawanyika wakitafuta njia ya kutokea.

Baada ya kutoka nje, baadhi ya waombolezaji hao wanadaiwa kuchukizwa hivyo kuanza kurusha mawe getini. Jeshi la polisi lilifika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwatawanya watu hao kwa kupiga risasi juu pamoja na mabomu ya machozi.

Radio alifariki baada ya kupata majeraha kichwani kutokana na ugomvi uliozuka katika bar moja mjini Entebbe.

Leo, maelfu ya mashabiki wa muziki wake wamejitokeza kumzika nguli huyo aliyeacha alama isiyofutika kwenye kiwanda cha muziki Afrika.

Nchemba: Kupambana na uhalifu sio lelemama
Dkt Nchemba aeleza Serikali inavyowaneemesha Polisi