Beki wa kati Chancel Mbemba amejiunga na mabingwa wa soka nchini Ureno FC Porto akitokea klabu ya Newcastle United, inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini England PL.

Beki huyo kutoka Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo alijiunga na Newcastle Utd akitokea Anderlecht ya Ubelgiji mwaka 2015, na aliitumikia klabu hiyo ya England katika michezo 59, ikiwepo michezo 11 ya msimu uliopita.

Newcastle Utd wamekubali kumuachia beki huyo mwenye umri wa miaka 23, huku wakiendelea kufanya siri makubaliao waliyofikia na uongozi wa FC Porto, japo baadhi ya vyombo vya habari vimekisia, huenda Mbemba ameuzwa kwa ada ya Pauni milioni 5.5 sawa na Euro milioni 7.20.

Kufuatia taratibu za uhamisho wake kukamilika, Mbemba anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha FC Porto kitakachocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Newcastle Utd mwishoni mwa juma hili.

Wakati Mbemba ameruhusiwa kuondoka, tayari meneja wa Newcastle Utd Rafael Benitez ameshakamilisha usajili wa wachezji watatu katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi ambao ni mlinda mlango Martin Dubravka aliyetokea Sparta Prague kwa ada ya Pauni milioni 4.5, kiungo Ki Sung-yueng aliesajiliwa kama mchezaji huru akitokea Swansea City pamoja na mshambuliaji wa pembeni Kenedy aliyetokea Chelsea kwa mkopo.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania, bado ana mipango ya kuongeza wachezaji wengine kwenye kikosi chake, kabla yakufungwa kwa dirisha la usajili mwanzoni mwa mwezi ujao.

Njombe yakabidhiwa vitabu 30,355 vya darasa la nne
Dawasco yawatahadharisha wakazi wa DSM kukosa maji siku ya kesho