Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Muhandisi Kashinde Mussa amewataka wasafirishaji wa mizigo wa magari kutokutumia nafasi ya akiba ya asilimia tano wanazopewa za kupakia mizigo ili kujiepusha na tatizo la mzigo kuzidi katika gari.

Ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Runinga ya Taifa TBC alipokuwa anazungumzia dhana ya uwepo wa mizani ya kupimia uzito, ambapo kwa Tanzania kuna mizani 64, yakudumu iliyojengwa kwenye maeneo ya kimkakkati nchini.

Amesema kuwa moja ya jukumu ya Wizara, ni kujenga barabara na kuziendeleza lakini pia kuzilinda ili kuhakikisha zinadumu kwa wakati uliokusudiwa na ndio maana wanalazimika kupima uzito wa magari ili kubaini magari yanayozidisha uzito wa mzigo.

Aidha Muhandisi Kashinde amesema endapo gari likibainika mzigo umezidi anachukuliwa hatua stahiki kwa kulipa tozo husika ya ya uharibifu wa barabara, lakini pia inampasa kupanga tena upya mzigo kwenye gari lake ili kuhakikisha unakaa sawa na kupimwa tena kwa mara ya pili.

Hata hivyo Muhandisi Kashinde amesema kuwa kupitia vituo hivyo 64 nchini wanaendelea kutoa elimu kwa watenda kazi katika vituo hivyo lakini pia hata kwa madereva ili kujiepusha na uharibu wa miundombinu za barabara.

KMC yaanika jeshi lake 2021/22
Naibu Waziri atoa onyo kwa maafisa ardhi