Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte anajiandaa kusaini mkataba wa awali wa kukinoa kikosi cha mabingwa wa soka nchini England Chelsea, baada ya kuthibitika jana aliwasili jijini Londan.

Conte ameonekana sehemu ya mitaa ya jiji la London, akifanya shughuli zake binafsi, lakini chanzo cha habari hizi kimeeleza kwamba, hii leo atakuwa na kikao na viongozi wa Chelsea kwa lengo la kusaini makubaliano ya awali huko Stamford Bridge.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46, anatarajia kusaini mkataba ambao utamuwezesha kulipwa mshahara wa paund million 15 kwa kila mwaka na atakaa magharibi mwa jijini London kwa kipindi cha miaka mitatu na endapo kazi yake itaridhisha atapewa nafasi nyingine ya kuwaongoza The Blues.

Chanzo cha habari kimeendelea kueleza kwamba, mazingira ya pande hizo mbili kukutana yamekuja baada ya Conte kuthibitisha ataachana na timu ya taifa ya Italia mara baada ya fainali za mataifa ya barani Ulaya za mwaka 2016 (Euro 2016), ambazo zitafanyika nchini Ufaransa.

Conte anatarajia kujenga upya benchi la ufundi la Chelsea na tayari imearifiwa atakuwa sambamba na ndugu yake wa damu Gianluca kama mshauri na makocha wasaidizi wametajwa kuwa ni Angelo Alessio, Massimo Carrera, Mauro Sandreani pamoja na mtaalamu wa mazoezi ya viungo Paolo Bertelli.

Wakati hayo yakiripotiwa kuwa hivyo, huko nchini Italia taarifa zinaeleza kwamba uongozi wa klabu ya AC Milan, nao umevutiwa na huduma ya Conte, na tayari umeanza harakati za kushawishi ili abakie nchini humo.

 

Picha: Jack Wilshere Aonekana Mitaani Usiku Wa Manane
Azam FC Waichunguza Esperance Hatua Kwa Hatua