Meneja wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Pablo Simeone, ametajwa kuwa katika mipango ya ajira kwenye klabu ya Chelsea ambayo kwa sasa inahaha kusaka matokeo mazuri kwenye mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini Engalnd.

Simeone, ametajwa katika harakati hizo, kutokana na meneja wa sasa wa Chelsea, Jose Mourinho kukalia kuti kavu, ambapo imedhihirika ameshindwa kuifanya kazi yake ipasavyo katika msimu huu wa ligi.

Meneja huyo kutoka nchini Argentina, amefikia hatua ya kutajwa katika ajira ya klabu ya Chelsea, kutokana na kazi yake nzuri anayoifanya kwenye klabu ya Atletico Madrid, ambayo kwa sasa imekua na mwenendo murua katika ligi ya nchini Hispania tena kwa kuzipa matumbo joto FC Barcelona pamoja na Real Madrid.

Hata hivyo haijadhihirika kama, kuna taratibu zozote ambazo zimeshaanza kufanywa na maafisa wa klabu ya Chelsea kwa ajili ya kumyakua meneja huyo, zaidi ya taarifa za Simeone kuandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

Wengine ambao wanatajwa kuwa katika chungu cha kumrithi Jose Mourinho endapo ataonyeshwa mlango wa kutokea huko Stamford Bridge, ni aliyekua meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers, Guus Hiddink pamoja na Carlo Ancelotti.

Mameneja hao watatu wote walishawahi kupita kwenye klabu ya Chelsea ambapo kwa upande wa Rodgers aliwahi kufanya kazi na Jose Mourinho kama msaidizi wake kati ya mwaka 2004–2007.

Guus Hiddink ambaye alitangaza kuitema timu ya taifa ya Uholanzi mwezi June mwaka huu kufuatia mambo kuwa magumu, aliwahi kufanya kazi kwenye klabu ya Chelsea kwa mkataba wa muda mfupi baada ya kutimuliwa kwa kocha Luiz Felipe Scolari katika msimu wa 2008–09.

Na Carlo Ancelotti aliwahi kuwa meneja wa kikosi cha Chelsea kuanzia mwaka 2009 hadi 2011 na alifukuzwa kazi kufuatia kukosa ubingwa wa England katika msimu wa 2010-2011.

CECAFA Senior Challenge Cup 2015 Mguu Sawa
Rais Magufuli Afanya Ziara Ya Kushtukiza Muhimbili