Klabu ya Chelsea imethibitisha kuwaacha baadhi ya wachezaji wake kutokana na sababu za mikataba yao kufikia tamati.

Mshambuliaji kutoka nchini Colombia Radamel Falcao, Alexandre Pato kutoka Brazil  pamoja na mlinda mlango Marco Amelia wa Italia wametajwa katika orodha ya wachezaji ambao hawatoendelea na klabu hiyo ya jijini London.

Falcao alijiunga na Chelsea kwa mkataba wa mkopo akitokea AS Monaco ya nchini Ufaransa, ameshindwa kuwashawishi viongozi wa The blues ili wamsajili moja kwa moja, kutokana na kiwango duni alichokionyesha msimu wa 2015-16.

Hata hivyo mshambuliaji huyo hakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na majeraha yaliyokua yanamkabili.

Naye mshambuliaji Alexandre Pato aliyesajiliwa kwa mkopo wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi januari mwaka huu, akitokea Corinthians anaingia katika mkumbo wa kushindwa kufikia vigezo vya kusajiliwa moja kwa moja hali kadhalika kwa mlinda mlango Amelia ambaye hakubahatika kucheza mchezo hata mmoja, licha ya kusajiliwa kwa kigezo cha kuziba nafasi ya Thibaut Courtois ambaye alikabiliwa na majeraha mwezi Oktoba mwaka jana.

Amelia alisajiliwa akitokea nchini kwao Italia katika klabu ya Lupa Castelli Romani inayoshiriki ligi daraja la pili.

Taarifa iliyotolewa kupitia tovuti  ya klabu ya Chelsea imeeleza kwamba mikataba ya mkopo ya wachezaji hao watatu, imefikia tamati na wameshapewa ruhusa ya kurejea katika klabu zao.

Mbali na kutoa uthibitisho huo, uongozi wa Chelsea umewashukuru wachezaji hao kwa kipindi chote walichokaa Stamford Bridge na umewatakia kila la kheri huko waendapo.

Joseph Omog Kutangazwa Rasmi Leo
Manchester City Wakamilisha Usajili Wa Nolito