Mbunge wa Bariadi Magharibi, Endrew Chenge ambaye jana amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bunge la 11, ameeleza hatua atakazochukua endapo sakata la Escrow alilohusishwa nalo litarudishwa mezani kujadiliwa.

Chenge alitajwa na kamati ya PAC chini ya uenyekitiwa wa Zitto Kabwe katika Bunge lililopita kuwa mmoja kati ya watuhumiwa waliofaidika na wizi wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta ESCROW.

Akijibu swali la Mbunge wa Ndanda kwa tiketi ya Chadema, Cecil Mwambe aliyetaka kujua kama mwanasiasa huyo mkongwe atakubali kusimamia mjadala wa sakata la ESCROW endapo litaletwa tena bungeni hapo akiwa kama mwenyekiti, Chenge alijibu kuwa ataheshimu kanuni za Bunge na kukaa pembeni na kuamuachia mtu mwingine aendeshe mjadala huo.

“Bunge letu linaongozwa na kanuni. Ikitokea kuna jambo linakuhusu unafuata kanuni. Unakaa pembeni na kumuachia mwingine achukue nafasi ili kuepuka Bunge kuwa na makandokando,” alijibu Chenge.

Chenge alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bunge pamoja Mbunge wa viti maalum, Dk. Mary Mwanjelwa na Najma Giga wote wa CCM.

Hotel ya Mtoto wa Amani Karume yateketea kwa moto, Vijana wawili wahusishwa
Faiza aburuzwa na matusi baada ya kupost video hii ya mwanae inayodaiwa kumdhalilisha 'SUGU'