Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amekiri kupokea kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zenye uhusiano na sakata la utakatishaji fedha na ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.

Akijitetea mbele ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili na Umma, Chenge alisema kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd kama malipo ya huduma ya ushauri wa kisheria aliyoitoa kwa kampuni hiyo.

Chenge alisema kuwa alisaini mkataba na kampuni hiyo ili kutoa ushauri wa kisheria katika mgogoro wake dhidi ya kampuni ya Mechmer ambazo zote ni kampuni binafsi.

Alisema kuwa haoni tatizo kufanya kazi hiyo kwa kuwa ni kazi binafsi ya kutumia taaluma yake na isiyohusiana na kazi yake ya utumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, Chenge alikana madai yaliyotolewa na Sekretarieti hiyo kuwa aliisababishia serikali hasara kwa kutoa ushauri wa kisheria ambao ulichangia kusainiwa kwa mkataba na Kampuni ya kufua umeme ya Indeependent Power Tanzania Limited (IPTL).

“Ninachofahamu mimi Serikali ndiyo imeingia mkataba na IPTL ambayo ilikuwa na asilimia 30 katika mkataba huo. Ni kweli mwaka 1995 nikiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi yangu ilipitia mkataba huo na kuridhia kwa sababu mikataba yote lazima ipitie pale, lakini sikuwa mimi binafsi kama Chenge niliyetoa ushauri wa kisheria kwa wizara ya Nishati na Madini,” Chenge ananukuliwa.

Chenge alipinga mara kadhaa nyaraka zilizokuwa zikiwasilishwa na Sekretarieti ya Maadili na Utumishi wa Umma na kudai kuwa vifungu vingi vya sheria vilikuwa vikitafsiriwa kimakosa.

“Katika kipindi ambacho nimeshangaa ni hiki. Nimefedheheka sana kuona watu wakitafsiri sheria za nchi tofauti na ambavyo zinamaanisha,” alisema Chenge na kusisitiza kuwa alizopata kupitia IPTL hakuzipata kama kiongozi wa umma bali alizipata kama mshauri wa kitaaluma.

Chenge aliitaka Sekretarieti kupuuza madai yaliyopo dhidi yake endapo upande wa mashtaka hautawasilisha ushahidi usiotiliwa shaka.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Sekretarieti hiyo, Katibu Msaidizi wa Idara ya Uongozi wa siasa, uchunguzi na maadili ya viongozi wa umma, Waziri Yahaya, alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa Serikali iliingia mkataba na IPTL kupitia Tanesco, wakati ambapo Andrew Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu Wa Serikali.

U23 Ya Nigeria Kuikabili Taifa Stars
Dzeko Aacha Majonzi Man City