Mshambuliaji kutoka nchini Mexico, Javier Hernandez ameendelea kumthibitishia meneja wa klabu ya Man Utd, Louis Van Gaal alikosea kumuacha mwanzoni mwa msimu huu.

Hernandez maarufu kama Chicharito, jana alifunga bao lake la 25 kwa msimu huu akiwa na klabu ya Bayer Leverkusen ya nchini Ujerumani hali ambayo imedhihirisha ana ubora kuliko washambuliaji wa sasa wa Man utd ambao hawajafikia idadi hiyo.

Chicharito ana mabao 11 zaidi ya mshambuliaji tegemezi wa Man Utd Wayne Rooney.

Chicharito alifunga bao lake la 25, dhidi ya FC Cologne ambao walikubali kulambishwa shubiri ya mabao mawili kwa moja ambapo bao lingine la kikosi cha Roger Schmidt lilifungwa na Julian Brandt.

Ushindi huo umeipeleka Bayer Leverkusen katika kundi la timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi ya nchini Ujerumani (Bundesliga) kwa kufikisha point 48 huku michezo mitano ikisalia kabla ya msimu wa 2015-16 haujafikia kikomo mwezi ujao.

Kama Bayer Leverkusen wataendelea kujiimarisha hapo ama kusonga katika nafasi za juu zaidi, watajihakikishia kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao wa 2016-17.

Wakati jitihada za Chicharito zikiiweka juu Bayer Leverkusen, Man Utd wamejiingiza katika ndoto za kufikirika, kufuatia kipondo cha mabao matatu kwa sifuri walichokipokea jana kutoka kwa Tottenham Hotspurs.

Kipigo hicho kimeiweka njia panda klabu hiyo katika harakati za ushiriki wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao, kwani kwa sasa Man utd wameendelea kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi ya nchini England kwa kufikisha point 53 wakitanguliwa na mahasimu wao Man City wenye point 57, zinazowaweka kwenye nafasi ya nne.

West Ham Utd wapo katika nafasi ya sita kwa kufikisha point 52, Southampton wana point 50 na Liverpool wapo kwenye nafasi ya nane kwa kufikisha point 48.

WAKURUGENZI WAWEKWA KITANZINI
Arsenal Walazimisha Mazungumzo Ya Usajili Wa Granit Xhaka