Bosi wa La-Familia, Chid Benz na wenzake watano wamewekwa chini ya uangalizi maalum wa mahakama na jeshi la polisi kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Chid na wenzake jana walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya upande wa Jamhuri kuiomba mahakama kuwaweka chini ya usimamizi maalum kwa kipindi cha miaka mitatu.

Polisi wa kituo cha Msimbazi waliwasilisha kiapo na kuiomba mahakama kuamuru wawekwe chini ya uangalizi maalum ikiwa ni pamoja na kusaini bondi na kuwa na wadhamini, ili kuhakikisha hawajihusishi tena na matumizi ya dawa za kulevya.

Chid na wenzake hawakuwa na pingamizi lolote kuhusu maombi hayo ya upande wa Jamhuri. Mahakama iliridhia maombi hayo na kuamuru msanii huyo na wenzake kuhakikisha wanaripoti katika kituo cha polisi cha Msimbazi mara moja kila mwezi kwa kipindi cha miaka miwili.

Aidha, kila mmoja alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao walitakiwa kusaini bondi ya shilingi milioni mbili kila mmoja.

Chid Benzi aliwahi kupandishwa kizimbani baada ya kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) miaka miwili mitatu iliyopita akiwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya kwenye mfuko wa shati.

Msanii huyo alikiri kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na amewahi kuhudhuria matibabu katika jumba maalum Bagamoyo (rehab). Hivi sasa amesema ameachana na matumizi ya dawa hizo zilizomuathiri kwa kiasi kikubwa.

Wabunge wa Maalim waondoka vichwa chini mahakamani
Serikali ya Zimbabwe yamkingia kifua mke wa Mugabe