Wachezaji wa klabu bingwa Tanzania bara Wekundu Msimbazi Simba wamezuiliwa kula vyakula vyenye mafuta na vinywaji vyenye sukari nyingi ili kulinda afya zao.

Amri hiyo kwa wachezaji wa Simba imetolewa katika kipindi hiki ambacho wachezaji wapo nyumbani, kufuatia janga la maambukizi ya virusi vya Corona, ambalo limesababisha shughuli za kimichezo kusimamishwa nchini Tanzania na kwingineko duniani.

Kocha Msaizidi wa Simba Seleman Matola, amesema wachezaji hawapaswi kula Chips na kunywa vinywaji vyenye sukari, jambo litakalolinda afya zao kwa sasa.

“Kuongezeka uzito kwa wachezaji inategemea na aina ya mfumo wa maisha, hivyo tumewashauri wasile baadhi ya vyakula visivyo na umuhimu,”

“Tunataka kumuona kila mchezaji akiwa katika mazingira mazuri kimwili, haitapendeza kuwaona wanarejea kambini wakiwa wameongezeka uzito, kama itakua hivyo tutaanza kuwanoa kwa program tofauti na tuliojiwekea, pindi ligi zitakaporuhusiwa kuendelea.”

Uongozi wa benchi la ufundi la Simba SC umetoa Program maalum kwa wachezaji wote, ambayo inatakiwa kufuatwa katika kipindi hiki cha kufanya mazoezi binafsi.

Ligi Kuu imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa alama zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

Corona kusababisha Condom kuwa adimu
Rage: Simba wakabidhiwe ubingwa