Moja kati ya matukio ya kihistoria ya mwaka 2014 yaliyozua zogo kubwa kila kona ni mvutano kuhusu umri wa Sitti Mtemvu, mshindi wa taji la Miss Tanzania 2014 aliyejivua taji hilo baada ya kugeuka kuwa taji la mwiba kwake.

Zogo hilo liliongezeka baada ya Hashim Lundenga, mkurugenzi wa Lino Agency ambao ni waandaaji wa shindano la Miss Tanzania alipoonesha cheti cha kuzaliwa cha Sitti Mtevu kilichobainisha kuwa mrembo huyo alizaliwa Mei 31 mwaka 1991 huku tarehe hizo zikikinzana na zile zilizokuwa kwenye hati yake ya kusafiria iliyokuwa ikionesha alizaliwa Mei 31 mwaka 1989.

Baada ya sakata hilo, serikali ilitangaza kulifungia shindano hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na kubainika kuwa na mapungufu mbalimbali.

Akiongea katika kipindi cha Nirvana cha Channel 5, ikiwa ni mara ya kwanza tangu ajivue taji la Miss Tanzania, Sitti Mtemvu alishindwa kuweka wazi uhalisia wa umri wake kwa sauti yake huku akieleza kuwa nyaraka zote mbili zilizoonesha umri wake kwa miaka tofauti ni za kwake.

Sitti alieleza kuwa hana sababu ya kueleza sasa hivi hadharani kuhusu umri wake kwa kuwa anataka mambo hayo yapite na aendelee na maisha yake.

“Hata nikisema nina miaka 20, 40 au 30 haitaleta utofauti.. kwahiyo nimeamua kufunga ukurasa. Hata nikisema tena hapa itafukua mambo yale ya zamani. Ndio maana nimewaandikia kitabu,” alisema Sitti.

Alimwambia mtangazaji wa kipindi hicho kuwa kama anapenda kufahamu yote kuhusu maisha yake ikiwa ni pamoja na umri wake basi akisome kitabu alichokiandika kwa kusaidiana na mwandishi mashuhuri, kinachoitwa ‘Chozi la Sitti’. 

Katika hatua nyingine, Sitti alikanusha taarifa kuwa aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Hashim Lundenga. Pia, alieleza kuwa taarifa za uongo juu yake kuwa alikuwa na mtoto zilimuumiza yeye na familia yake kwa kuwa mtoto aliyekuwa anatajwa ni mdogo wake.

Alisema kuwa asingependa mrembo yeyote apitie mambo aliyoyapitia katika sakata hilo kwani yalimuumiza yeye na familia yake nzima kutokana na matumizi ya jina lake.

 

Mtoto wa Karume amshauri Dk. Shein Ampishe Maalim Seif
Ni Mzunguuko Wa Tatu Wa Kombe La Shirikisho