Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Chris Mugalu, amewashukia baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wanaoendelea kumlaumu na kumtukana kupitia mitandao ya kijamii, kufuatia changamoto ya kushindwa kufunga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans.

Baadhi ya Mashabiki wa Simba SC wamekua wakimlaumu Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo, kwa kusema hakujituma ipasavyo kwenye mchezo huo, ambao ulimalizika kwa Young Africans kupata ushindi wa bao 1-0.

Mashabiki hao wamemtupia lawana Mugalu kwa kusema alikua sababu ya kikosi chao kushindwa kufikia lengo la kufunga bao la kusawazisha na kuongeza bao la ushindi kwenye mchezo huo, ambao ulishuhudia Young Africans wakitwaa Ngao ya Jamii.

Mugalu amewajibu wanaomlaumu na kumtusi, kwa kuandika ujumbe kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, kwa kuamini njia hiyo itawezesha ujumbe wake kuwafikia wote wanaoendelea kumbeza.

“Je ! haitoshi kwako kuwa mnafiki na kutukana wakati ninashinda ubingwa, unasema mimi ndiye bora, na nikishindwa, unanitukana ? Unafiki unatosha kwako” ameandika Chris Mugalu

Msimu uliopita 2020/21 Mugalu alimaliza katika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora, baada ya kufunga mabao 15 akitanguliwa na Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC John Raphael Bocco aliyemaliza na mabao 16.

ALAT yaja na neema kwa madiwani
Taifa Stars yatajwa, kucheza ugenini Oktoba 07