Sakata la mgogoro wa Uenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliopashwa joto na aliyekuwa mwenye ‘kiti’ hicho, Profesa Ibrahim Lipumba umeendelea kuibua mapya na kufunua mengine yaliyopita kama siri ya chama.

Siku chache baada ya Profesa Lipumba kusikika kupitia Clouds Fm akieleza kuwa ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa ndio chanzo cha yeye kujivua Uenyekiti akidai kuwa hakushirikishwa na kwamba mwasiasa huyo hakufaa kupewa nafasi hiyo, amesababisha Uongozi wa CUF kutoa siri ya mpango wa mwanasiasa huyo kwa Jaji Joseph Sinde Warioba.

Jaji Joseph Warioba

Jaji Joseph Warioba

Akijibu tuhuma zilizotolewa na Profesa Lipumba dhidi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa aliendesha kikao cha kumpokea Lowassa bila kumshirikisha, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa CUF, Mbarara Maharagande alieleza kuwa Lipumba alifanya kazi ya kumshawishi Jaji Warioba kugombea urais kupitia Ukawa.

“Alichokuwa anafanya Maalim Seif ni haki ya Kikatiba kushirikiana na viongozi wengine wa Ukawa. Mbona yeye [Lipumba] alikuwa anamfuata Mzee Joseph Warioba kumshawishi agombee urais?” Maharagande anakaririwa.

Jaji warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu, alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambapo kupitia mchakato wa mabadiliko ya katiba vyama vya upinzani viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaounga mkono rasimu ya katiba.

Profesa Lipumba ambaye Baraza Kuu la CUF limemsimamisha uanachama yeye pamoja na viongozi wengine 10, ameendelea kudai kuwa yeye ndiye Mwenyekiti halali wa chama hicho kwakuwa alijiuzulu kabla ya uchaguzi lakini ameandika barua ya kutengua uamuzi wake wa awali.

Lipumba amesikika akimshambulia Lowassa kuwa ameinunua CUF kwa bei chee na kwamba hataruhusu hicho kitokee akiwa nje ama ndani ya chama hicho.

Kauli hizo za Lipumba zimewaacha wengi mdomo wazi kwani ndiye aliyeongoza kikao cha kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa mbele ya waandishi wa habari na kumsaidia kujibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa kuhoji uadilifu wake.

Malawi yadaiwa kuichokoza tena Tanzania kuhusu Ziwa Nyasa
Wakuu wa Mikoa Kanda ya ziwa waeleza madhara ya tetemeko la ardhi lililoleta maafa