Serikali imeliagiza Baraza la hifadhi ya Mazingira Nchini (NEMC ), na Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais kufanya tathimini ya awali ya kuangalia ni namna gani itaweza  kuzuia maji ya bahari kuingia katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa)  na kuharibu miundombinu yake ambapo hadi sasa takribani mita 70 hadi 100 ya maji ya bahari yameisogelea Taasisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina, alipofanya ziara Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, amesema kutokana na hali hiyo kuwa ya dharura ameziagiza mamlaka hizo kufanya tathimini ya awali ambapo amewataka kufikia Januari 30 mwakani kukabidhi ripoti ya awali kwa Serikali na ili kujua kifanyike katika kunusuru taasisi hiyo na kuifanya mahala pazuri pa kujifunzia masuala ya utamaduni.

Mpina amesema ripoti hiyo itapelekwa Serikalini ili mipango madhubuti  ianze kufanyika ya kuhakikisha taasisi hiyo  inaendelea kutoa mafunzo yake kama kawaida bila kuathiriwa na usogelewaji wa bahari katika maeneo hayo.

“Januari 30 mwakani tutapata hiyo ripoti na kuipeleka Serikalini na kuangalia ni namna gani tutakavyonusuru taasisi hiyo na kama kutahitajika utafiti mwingine wa kina kuhusiana na jambo hili,utaweza kufanyika na kujua nini  kifanyike katika maeneo haya kama kutengeneza Makinga maji au Ukuta,”alisema Mpina

Aidha, Mpina amesema kuwa hali ya bahari kuhamia katika maeneo ya nchi kavu  inatokana na kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi yanayotokea baharini ambapo kwa sasa  kina cha bahari kimeweza kuongezeka kufikia Sentimita 19 na kusababisha madhara ya maji kusogea katika maeneo ya nchi kavu.

Hata hivyo, Mpina amesema mpaka sasa kuna  baadhi ya fukwe tayari zimeanza kufanyiwa utaratibu wa kujengwa kwa kingo zikiwemo fukwe za Pangani Tanga, Kilimani Zanzibar, Kisiwapanza Pemba, pamoja na fukwe za Ocean road Dar es Salaam.

 

Waziri awasha moto TASAF, atumbua maofisa waandamizi wa mfuko huo
Majaliwa aibana NCAA, ataka nyaraka za Faru John ifikapo Desemba 8, 2016