Chuo kikuu cha Dar es salaam UDSM wameshauriwa kutumia maadhimisho ya miaka 55 tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto walizokumbana nazo katika kipindi kilichopita ili kujiwekea malengo ya maendeleo ifikapo 2061.

Hayo yamesemwa na  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa  katika hafla ya kufunga maadhimisho ya  miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika katika ukumbi wa Nkurumah leo Jijini Dar es Salaam.

“Leo ni siku ambayo tunahitimisha Maadhimisho ya miaka 55 tangu kuanzishwa kwa Chuo hiki, ni vyema basi tukatumia sherehe hizi kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto mlizokumbana nazo kwa kipindi kilichopita”. Alisema Majaliwa.

Awali akisoma hotuba yake Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuelezea namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga kuhakikisha inafanya maboresho makubwa katika taasisi za elimu za umma ikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amezitaja baadhi ya changamoto na namna ambavyo Serikali imekuwa ikizishughulikia kuwa ni pamoja na; Maslahi ya watumishi, wanataalamu na waendeshaji ambapo alisema Serikali inatambua uwepo wa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, na kuongeza kuwa suala hilo tayari limekwisha anza kushughulikiwa kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo zoezi la uhakiki wa wafanyakazi na watumishi hewa.

Kuhusu changamoto ya uhaba wa Wahadhiri Waandamizi na Maprofesa katika Vyuo vya Umma, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo na kuvitaka Vyuo navyo viweke taratibu na mipango endelevu ya kurithishana ili kupunguza ombwe lililopo.

Akizungumzia kuhusu mikopo ya Elimu ya Juu, Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Serikali kupitia Rais Dkt. John Pombe Magufuli  imetoa ufafanuzi wa namna utekelezaji wa kutoa mikopo hiyo, na Wizara yenye dhamana inaendelea na uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo. Alitoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe wanawasilisha taarifa sahihi na za uhakika.

Nakuongeza kuwa Serikali imekwisha ongeza bajeti ya mikopo ya Elimu ya Juu kutoka shilingi bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017 hivyo hakuna mwanafunzi anyestahili kupata mkopo atakayekosa.

Awali akisoma historia ya chuo hicho Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa maadhimisho hayo wanayatumia kufanya tathmini ya safari ya Chuo kuelekea maendeleo ya karne moja ifikapo mwaka 1961.

Profesa Rwekaza amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa katika ukuaji wa Chuo hicho uliotokana na mahitaji kulingana na wakati husika na kuongeza kuwa lengo kubwa la uongozi ni kuhakikisha Chuo hicho kinaendela kuwa kinara katika kutoa elimu bora kulingana na wakati.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto kadhaa walizokumbana nazo Chuo hicho kimekuwa daraja muhimu la kuzalisha wanataaluma ambapo takribani wanataaluma 90,000 wa ndani na nje ya nchi wametokana na chuo hicho.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Joyce Ndarichako amesema kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.

Amesema kuwa wizara imekuwa ikiendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhudumia sughuli mbalimbali za maendeleo ya elimu na kuongeza kuwa hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni ambao unatarajiwa kukamilima ifikapo Desemba 2016.

Mradi huo utakapokamilika  utapunguza changamoto ya uhaba wa mabweni kwa wanafunzi na kuwaondolea hadha ya kuishi mitaa, huku mabweni hayo yakitarajiwa kutumiwa na wanafunzi takribani 3840.

Chuo kikuu cha Dar es Salaa kinaadhimisha miaka 55 tangu kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1961 huku kikianzia katika majengo ya TANU( sasa hivi CCM) yaliyoko mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika eneo la Mlimani mnamo mwaka 1964.

EFL Yazidi Kuchanja Mbuga, Tano Zatangulia Robo Fainali
Picha: Mfalme Mohamed VI wa Morocco aweka jiwe la msingi ujenzi wa msikiti