Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama amekwenda kinyume na Mashabiki wa Simba SC ambao walionesha kukasirishwa na maamuzi ya kutolewa kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, juzi Jumatano (Januari 18).

Kocha Robertinho alimtoa Chama dakika ya 32, na nafasi yake ilichukuliwa na Kiungo Mshambuliji Kibu Denis, hali ambayo ilizua taharuki kwa Mashabiki ambao hawakupendezwa na mabadiliko hayo.

Akizungumza baada ya malalamiko hayo kuchukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii jana Alhamis (Januari 19), Chama amesema anaheshimu maamuzi ya Kocha Robertino na amefurahi Simba SC kushinda dhidi ya Mbeya City.

Amesema kipaumbele cha Simba SC ni kushinda na kila mtu kuwa na furaha, hata yeye alifurahia kilichotokea baada ya dakika 90, hivyo mengine ambao yanaendelea kuzungumzwa kuhusu kutolewa hayana umuhimu kwake.

“Ni furaha kuona timu imepata matokeo na hilo ndio la msingi zaidi, ndio kipaumbele kwa kila mtu ambaye yupo hapa Simba SC, sio Wachezaji, Kocha wala Viongozi na hata Mashabiki.”

“Wote lengo letu ni moja yaani kuhakikisha na kuona timu inashinda, hivyo nimefurahi sana kwa kupata matokeo mazuri, hayo mengine ambayo yamejitokeza wala hayana umuhimu sana.” amesema Chama

Msimu huu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara Chama amecheza michezo 17 akifanikiwa kufunga mabao matatu na kutoa pasi za mwisho 12.

Fiston Meyele amkosha Kennedy Musonda
Leandro Trossard kupima afya London