Mlinda mlango wa klabu ya Man City Claudio Bravo, amepatwa na majeraha akiwa katika shughuli ya utetezi wa taifa lake la Chile, jambo ambalo huenda likawa limeibua hofu kwa meneja Pep Guardiola.

Bravo alionyesha kiwango cha hali ya juu wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Colombia kwa kupangua mipira iliyokua imeelekezwa langoni mwake, kabla ya kupatwa na majeraha ya mguu.

Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, ulishuhudia mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 33, akitolewa nje katika dakika ya 64, na nafasi yake kuchukuliwa na Johnny Herrera.

Mpaka sasa shirikisho la soka nchini Chile halijatoa taarifa za maendeleo ya mlinda mlango huyo wa kutumainiwa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo.

Kikosi cha Chile kitarejea tena dimbani kati kati ya juma lijalo kucheza mchezo mwingine wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya timu ya taifa ya Uruguay, huku Colombia wakitarajia kuwa wageni wa Argentina.

Argentina Yaangukia Kidevu Belo Horizonte-Brazil
Fabio Capello Afichua Siri Ya Kuikataa The Azzurri