Meneja mpya wa klabu ya Fulham inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini England Claudio Ranieri, amesisitiza kufahamu vyema mbinu za kuepuka kushuka daraja.

Ranieri ambaye alitangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London Novemba 14 kufautia kutimuliwa kwa Slaviša Jokanović, amesisitiza jambo hilo kutokana na hali aliyoikuta klabuni hapo, ambapo mpaka sasa Fulham inakamata nafasi ya 20 huku ikiwa na alama tano, baada ya kushuka dimbani mara 12.

Meneja huyo kutoka nchini Italia amesema, sio mara ya kwanza kukabidhiwa klabu ikiwa katika hali mbaya, kwani aliwahi kukubali jukumu hilo mara kadhaa na alifanikiwa kufikia lengo.

“Wakati ninaajiriwa na uongozi wa klabu ya Parma ya nyumbani kwetu Italia, ilikua mwishoni mwa mwezi Februari, hali ilikua kama niliyoikuta hapa, nilipambana na nilifanikiwa kuibakisha timu kwenye ligi ya Serie A,” Alisema Ranieri alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Fulham.

“Nina uhakika kila mtu ameshangazwa na maamuzi nilioyachukua, lakini ninajua nini nitakacho kifanya hadi kufikia lengo la kuiona Fulham inafanya vyema na kumaliza msimu ikiwa kwenye nafasi salama,”

“Mtihani mwingine niliowahi kuupitia na nikafanikiwa, nilipokua na klabu ya Cagliari, nakumbuka nilipewa kazi ya kuifundisha ikiwa kwenye ligi daraja la tatu Italia Serie C, lakini kila msimu nilifanikiwa kuipandisha daraja, tulicheza Serie B na msimu watatu tulipanda ligi kuu (Serie A), binafsi ninapenda sana mitihani kama hii, ili kuudhihirishia ulimwengu hakuna linaloshindikana, unapoweka malengo.”

“Ninaamini nitafanya kazi kwa kushirikiana na kila mmoja ili nifanikiwe katika zoezi hili la kuifikisha mahala pazuri Fulham. Haitokua kazi rahisi, lakini nitaweza na kila mmoja ataona nitakachokifanya.”

Hii si mara ya kwanza kwa Ranieri kufundisha soka nchini England, kwani aliwahi kufanya kazi na Chelsea kuanzia mwaka 2000–2004, na baadae alirejea kuinoa Leicester City kuanzia mwaka 2015–2017.

Akiwa na Leicester City alifanikiwa kuiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa England msimu wa 2016/17.

Matteo Guendouzi afunguka kuhusu Arsenal
Wapenzi watiwa mbaroni kwa kughushi cheti malipo ya korosho