Meneja wa klabu bingwa nchini England Leicester City Claudio Ranieri, amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kufanya kazi na uongozi wa klabu hiyo hadi mwaka 2020.

Ranieri amejitia kitanzi kwa kusaini mkataba huo, kufuatia mafanikio aliyoyavuna klabuni hapo msimu uliopita, ambapo aliiwezesha Leicester City kutwaa ubingwa wake wa kwanza katika historia ya soka ya soka nchini England.

Baada ya kukamilisha mpango huo, meneja huyo kutoka nchini Italia alisema imekua faraja kwake kuendelea kubaki klabuni hapo tena kwa nguvu ya viongozi ambao wameonyesha kukunwa na mafanikio aliyowaletea msimu uliopita.

“Nilizungumza na uongozi na umeniambia nini mustakabali wa Leicester City kwa siku za usoni, hivyo ninajua nimefanya maamuzi sahihi ya kuendelea kubaki klabuni hapa.

“Natumai mambo mazuri yataendelea kupatikana kwa ushirikiano na viongozi wangu ambao wameonyesha kuwa bega kwa bega nami, hivyo sina wasiwasi wa kuendelea kufanya kazi kwa lengo la kutafuta mafanikio mengine kwa kipindi cha miaka minne kama mkataba wangu unavyoelekeza.” Ranieli amenukuliwa na tovuti ya klabu ya Leicester City.

 

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 64, alibadilisha mawazo ya mashabiki walio wengi duniani kote baada ya kushindwa kupewa nafasi ya kufanya vyema alipotangazwa kuwa meneja wa Leicester City mwanzoni mwa msimu uliopita, kutokana na klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ya nchini England msimu wa 2014/15. Kwa upande wa makamu mwenyekiti wa Leicester City Aiyawatt Srivaddhanaprabha ameongeza kuwa: “Miaka 12 iliyopita, tulimtambulisha Ranieri kwa waandishi wa habari na tulitambua uwezo wake, tulijiamini na kuwapuuza waliotubeza kwa maamuzi yetu, na mwishoni mwa msimu uliopita ilidhihiri nini tulichokua tumekitarajia.” Tovuti ya Leicester City imeandika.


Leicester City (The Foxes) wanatarajia kushiriki kwa mara ya kwanza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2016/17 na huenda wapangwa na timu za Borussia Dortmund, Atletico Madrid pamoja na Sevilla.

Matarajio hayo yanatokana na kanuni mpya za upangaji wa makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambapo mabingwa wa nchi husika hupangwa katika chungu A (Pot 1), hatua ambayo inawatenganisha na mabingwa wa nchi nyingine kama FC Barcelona, Bayern Munich pamoja na Real Madrid.

Azam FC Kucheza Mchezo Wa Kimataifa Wa Kirafiki
Nyambizi Ya Manjano Yapata Pigo, Majibu Kutoa Mustabali