Meneja wa klabu bingwa nchini England Leicester City, Claudio Ranieri amesisitiza kuwa, kiungo wake kutoka nchini Algeria Riyad Mahrez atabakia King Power Stadium licha ya kuhusishwa na mipango ya kutimkia Arsenal.

Ranieri alihojiwa na Wanahabari baada ya mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Oxford waliokubali kufungwa mabao 2-1, kuhusu tetesi za Riyad Mahrez kuhamia Arsenal, alikata kata kata kwa kusema kiungo huyo haendi popote.

“Kila Mtu hapa ana furaha. Na Mahrez anataka kubaki. Hakuna Mchezaji mwingine ataondoka. Tutabaki wote pamoja!”

Mahrez, ambaye msimu uliopita aliisaidia Leicester City,  kutwaa ubingwa wa England kwa mara ya kwanza sambamba na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa chama cha wachezaji wa kulipwa PFA, amekua akihusishwa na taarifa za kuwindwa na klabu za Barcelona, Arsenal na Manchester City.

Hivi karibuni, Leicester  City walifanikiwa kumshawishi mshambuliaji wao kutoka nchini England, Jamie Vardy ambaye tayari ofa yake ilikua imeshatua King Power Stadium kutoka kwa Arsene Wenger.

Mwishoni mwa juma lililopita, Leicester City walikubali kumuachia kiungo wao kutoka nchini Ufaransa, N’Golo Kante ambaye alijiunga na klabu ya Chelsea.

Kwenye Mchezo wa Jana, Oxford walitangulia kupata bao la kuongoza kupitia Chris Maguire aliyepiga mpira wa adhabu ndogo ulioelekea moja kwa moja langoni mwa The Foxes, lakini Leicester City walipambana na kufanikiwa kupata ushindi wa mabao mawili yaliyofungwa na Demarai Gray na Jeffrey Schlupp.

Katika mchezo huo, Ranieri aliwachezesha kwa mara ya kwanza wachezaji aliowasajili katika majira haya ya kiangazi Ron-Robert Zieler, Luis Hernandez na Ahmed Musa sambamba na kuwatumia chipukizi kutoka kikosi cha pili cha Leicester City Admiral Muskwe na Hamza Choudhury.

Didier Drogba: Hakuna Zaidi Ya Cristiano Ronaldo
Video: Kiwanda cha Pepsi Kulipa Faini ya Milioni 25 Kwa Uchafuzi wa Mazingira