Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, leo Al-Khamis watashuka dimbani kuwakabili Coastal Union, Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga katika mzunguuko wa 37.

Simba SC watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao mawili kwa sifuri waliopata dhidi ya wenyeji wao Coastal Union katika mchezo wa mzunguko wa kwanza huku mchezo uliyopita dhidi ya Alliance FC waliondoka na ushindi mnono wa mabao matano kwa moja.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema kikosi chake kiko katika hali nzuri na wanahitaji kuendeleza kasi ya ushindi katika ligi hiyo ambayo sasa ‘vita’ yake imebakia kwa timu zinazopambana kujiepusha na janga la kushuka daraja.

Sven amesema hakuna mchezo rahisi katika Ligi Kuu ingawa leo anakutana na timu isiyokuwa na presha ya aina yoyote kwa sababu iko mahali salama.

Mbelgiji huyo amesema anahitaji kuona wachezaji wake wanajituma katika mchezo huo ili kuendelea kujiimarisha na kujiweka tayari na mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la FA inayowasubiri.

“Ni mchezo utakaokuwa na burudani na mambo mengi ya kiufundi, kila timu itaingia uwanjani bila mawazo, sisi tayari ni mabingwa na wenzetu hawana cha kupoteza, wote tunahitaji heshima kwa mashabiki wetu pia, kila siku hakuna anayependa kuona timu yake inafungwa,” alisema Sven.

Kocha huyo aliongeza ataendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wake ambao hawakupata namba katika michezo iliyopita ili kuitumikia timu yao kwenye hatua hii ya lala salama.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda, amesema wamejipanga kusaka ushindi katika mechi ya leo na kumaliza ‘uteja’ dhidi ya mabingwa hao wa Bara.

Alisema kila mchezaji anafahamu wamekuwa na matokeo mabaya dhidi ya Simba kwa msimu wa pili na leo wanataka kufuta ‘unyonge’ waliokuwa nao kwa muda mrefu.

“Tumekuwa na bahati nzuri tukiwa Mkwakwani, naamini kesho (leo), wachezaji wangu hawataniangusha, kama watafuata tunayoyafanya mazoezini, tutaishangaza Simba, ila wanajua kwetu huwa si mteremko,” Mgunda alisema.

Michezo mingine ya mzunguuko wa 37 Ligi Kuu itakayochezwa leo ni kati ya Polisi Tanzania dhidi ya JKT Tanzania wakati Lipuli itawakaribisha Ruvu Shooting, huku Ndanda ikiwafuata Alliance na Azam FC itavaana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini, Dar es Salaam.

PICHA: Liverpool wakabidhiwa kombe la Ubingwa EPL
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 23, 2020