Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Twaha mwishoni mwa juma lililopita amekutana na kamati ya utendaji ya klabu hiyo ili kujua tatizo linalowakwaza, hadi kufikia hatua ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Twaha, alifikia hatua ya kukutana na viongozi wenzake, baada ya kushauriwa na baadhi ya wanachama ambao walikua wanahisi huenda kuna mambo yanashindwa kuwekwa sawa klabuni hapo, hali ambayo inasemekana kuwa chanzo cha upepo wa klabu kutokwenda vizuri.

Afisa habari wa Coastal Unon Oscer Assenga amezungumzi na Dar 24.com, na kuthibitisha kufanyika kwa kikao hicho, lakini akashindwa kueleza kwa undani nini kilichozungumzwa kwa kina.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Twaha akiwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ya jijini Tanga

Assenga, amesema maazimio ya kikao hicho huenda yakatolewa katika vyombo vya habari kuanzia kesho asubuhi, japo akagusia kidogo suala la kutokufanya kwao vizuri katika michezo ya ligi kuu.

“Suala la kikosi chetu kutokufanya vyema katika michezo ya ligi kuu nalo limezungumzwa, lakini ningependa kukuhakikishia kesho kila jambo litawekwa bayana” Alisema Assenga.

Coastal Union, imeonyesha udhaifu mkubwa katika mshike mshike wa ligi kuu msimu huu, na baada ya kufungwa katika mchezo wao wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Simba mabao mawili kwa sifuri, kumewafanya kuburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo.

Kwa sasa Coastal Union wanamiliki point 19, ikiwa ni tofauti ya point moja dhidi ya ndugu zao African Sports na Mgambo JKT wenye point 20 kila mmoja.

Tanzia: Msafara wa Kamati ya Bunge wapata ajali, watano wafariki
Assah Mwambene ang'olewa Idara ya Habari Maelezo