Klabu ya Coastal Union yenye maskani yake makuu jijini Tanga, imetoa taarifa ya usajili wa wachezaji ambao wataitumikia klabu hiyo msimu wa 2020/21, ambao umepangwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.

Coastal Union wametoa taarifa hiyo, baada ya TFF kutangaza kufunguliwa kwa dirisha la usajili kuanzia leo Agosti Mosi hadi Agosti 31, ili kutoa nafasi taratibu nyingine kufuatwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu.

Uongozi wa klabu hiyo umesema hauna wasiwasi wowote kutokana na tetesi za nyota wake waliokisaidia kikosi hicho kufanya vema msimu huu, kutakiwa na klabu nyingine zikiwamo Simba SC na Young Africans.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto, amesema hawana presha kwa sababu wana benchi la ufundi imara ambalo linaweza kuwatengeneza wachezaji wengine na timu yao ikaendelea kufanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mguto amesema tetesi hizo wamezisikia lakini watawaruhusu wachezaji wao kuondoka baada ya klabu zinazowahitaji kukubali kuwalipa kiasi cha fedha wanazotaka.

Kiongozi huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi Ya Ligi Tanznaia Bara (TPLB) amesema hawatamzuia mchezaji yoyote kuondoka kama klabu inayomhitaji itakubali kumpatia maslahi bora kwa ajili ya kuendeleza kipaji cha mchezaji husika pamoja na wao ambao wamemkuza nyota huyo.

“Viongozi tulikutana na kujadili suala hilo baada ya kusikia na kuona tetesi juu ya wachezaji wetu, kwa sasa tunachokisubiri ni ripoti ya kocha wetu (Juma Mgunda), tutaangalia wachezaji ambao wanabaki na wale ambao wanaondoka, iwe kwa sababu ya kutakiwa na timu nyingine, halafu tutaanzia hapo.”

Mguto akaongeza kuwa wamepanga kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema na hivyo wamemtaka Mgunda kuwasilisha ripoti yake mapema ili ifanyiwe kazi kwa ufanisi.

NEC yatoa maelekezo kwa wasimamizi Uchaguzi mkuu
Fainali ASFC: Matola, Hitimana watambiana

Comments

comments