Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja Mkandamizaji ameeleza jinsi alivyohojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Dodoma ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Patrobas Katambi.

Mkuu wa wilaya hiyo alimtaka Masanja kufika katika kituo cha polisi au ofisini kwake mara moja baada ya kurusha maudhui ya ucheshi akiwahoji baadhi ya wakaazi wa jiji la Dodoma kuhusu virusi vipya vya corona (covid-19). Mchekeshaji huyo alirusha maudhui hayo yakiwa na watu ambao walikosea majibu pekee.

Akizungumza jana mbele ya waandishi wa habari akiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Masanja alisema kuwa alihojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, alitoa sababu za kurusha maudhui hayo huku akisisitiza kuwa dhamira yake ilikuwa njema ingawa matokeo yalikuwa makosa.

Hata hivyo, Masanja anasema baada ya kuelezwa na kupitishwa kwenye vifungu vya sheria alielewa kuwa alifanya makosa, na akaomba msamaha ambao ulikubalika na akasamehewa.

Alimshukuru DC Katambi kwa kuchukua hatua ya kukemea kwa haraka kitu ambacho alikiona hakikwenda sawa kwenye mkoa wake, akieleza kuwa akili ya kijana huenda kasi katika kufikiri madhara na ndivyo alivyofanya.

Alisema baada ya kikao hicho ameambiwa yuko huru kurudi jijini Dar es Salaam na ataendelea kutoa elimu mtaani na kanisani kuhusu virusi vipya vya corona (covid-19).

Makonda kuwakamata wanaozurura mjini kuepuka corona
Limao katika mwili wa binadamu huongeza kinga ya mwili

Comments

comments