Beki wa kati kutoka nchini Brazil Gabriel Armando de Abreu, amechimba mkwala kwa kusema hatokubali kurejea uwanjani akiwa na klabu yake ya Valencia ya Hispania, bila uwepo wa chanjo ya virusi vya Corona (Covid-19).

Beki huyo wa zamani wa klabu ya Arsenal ya England, ameleza wasiwasi wake juu ya kurudi kwa ligi za soka duniani, lakini akasisitiza kuwa ni vyema ligi zikarejea ikiwa tayari chanjo ya ugonjwa huo ikiwa imepatikana.

Gabriel Paulista amesema anahitaji kuhakikishiwa kwa asilimia 100, kama ligi ya Hispania na ligi nyingine zitakaporejea, chanjo itakua imeshapatikana, ama mpango wa kurudisha ligi unaendelea kusukwa bila ya kufahamu ni lini suluhisho litapatikana.

“Wachezaji wa mpira wa miguu ni watu kama wengine kwenye jamii, tuna familia, ndugu na marafiki na tuna hisia, sitapendezwa kuona tunarejea uwanjani tukiwa katika hali ya sintofahamu kuhusu chanjo.”

“Tunahitaji kuweka mfano kwa jamii kuwa tunathamini maisha na afya kuliko kitu chochote, kila mchezaji anapaswa kuwa na msimamo ili kuionyesha dunia, ni namna gani tunavyopaswa kuwa makini.”

“Kwangu, na nina uhakika kwa idadi kubwa ya wachezaji, pesa sio kila kitu, hapa tunazungumzia maisha ya watu, tusifanye mzaha na afya za watu kwa kuangalia faida ya muda mfupi.”

“Ninapenda soka, napenda kucheza, napenda klabu yangu na kila wakati ninataka kufurahisha mashabiki, lakini zaidi ya yote, napenda na ninaheshimu maisha ya kila mwanadamu.”

“Tunahitaji kucheza wakati hakuna tena hofu na wakati tuna uhakika kamili kuwa hakuna Coronavirus.” Amesema Gabriel Paulista.

Paulista alisajiliwa na Valencia mwaka 2017 akitokea Arsenal, na tayari ameshaitumikia klabu hiyo ya Estadio Mestella katika michezo 117 na kufunga bao moja.

Akiwa Arsenal kuanzia mwaka 2015–2017 alicheza michezo 46 na kufunga bao moja, Villarreal ya Hispania kuanzia mwaka 2013–2015 alicheza michezo 50 na kuanzia mwaka 2010-2013 alicheza klabu ya Vitória ya kwao Brazil.

Corona: Waziri aagiza Mkurugenzi Maabara ya Taifa asimamishwe kazi
Mwanafunzi miaka 9 abadilika rangi kwa maradhi ya moyo, aomba msaada