Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza shule za awali, msingi na sekondari kufungwa kwa siku 30 kama hatua ya kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu pia amesema Serikali imesitisha michezo yote inayokutanisha makundi ya watu.

“Tumesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama Ligi Kuu, Ligi daraja la kwanza na la pili, michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA na ile ya mashirika ya umma kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo”- Amesema waziri mkuu Kassim Majaliwa,” amesema Waziri Mkuu.

Hatua hiyo imetangazwa ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutangaza kisa cha kwanza cha corona, ambapo mwanamke mmoja Mtanzania mwenye umri wa miaka 46 alibainika kuwa na virusi vya corona. Mgonjwa  huyo aliingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), akitokea nchini Ubelgiji.

Akizungumzia hatua ambazo Serikali imezichukua, Waziri Mkuu alisema Serikali imemhifadhi mwanamke huyo kwenye eneo maalum kwa ajili ya kumpa huduma za kitabibu.

“Serikali imefanya ufuatiliaji wa watu waliokutana na mgonjwa huyo na kuwaweka kwenye karantini kwa siku 14, na pia kuchukua sampuli kubaini kama wameathirika,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza kuwa Serikali itaimarisha uwezo wa kuchukua sampuli na kwamba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ina uwezo wa kupima na kutoa majibu kwa haraka.

Aidha, alisema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa wizara ya afya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, lakini pia imetenga maeneo maalum kwa ajili ya karantini.

“Serikali imetenga Hospitali maalum za Mloganzila (Dar es Salaam), Kituo cha Busweru (Mwanza), Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibar), Chakechake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu pia ameeleza kuwa Serikali imeshatoa Sh 500 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru ili zitumike katika kuwezesha mapambano dhidi ya virusi vya corona, kama alivyoagiza Rais John Magufuli.

CORONA: EURO 2020 yapelekwa 2021
CORONA: TFF waitana kwa dharura