Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameagiza Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuitisha kikao cha dharula kesho kujadili mustakabali wa michuano hiyo wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona.

Karia amesema kwamba kikao hicho kitakachoanza Saa 3:00 asubuhi kitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam.

“Ajenda kubwa katika kikao hicho ni kuangalia mustakabali wa ligi kutokana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona ambao umeingia nchini,”amesema Karia.

Tayari Ligi mbalimbali duniani, ikiwemo michuano ya Afrika imesimamishwa kwa hofu ya maambukizi ya ugonjwa huo hatari.

Na leo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa tamko la kuahirisha fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon.

Na hiyo ni baada ya CAF kuahirisha mechi za tatu na za nne za kufuzu Fainali za Kombe za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 baina ya Tanzania na Tunisia zilizokuwa zifanyike mwishoni mwa mwezi huu Tunis na Dar es Salaam zimeahirishwa.

Kwa ujumla CAF imesimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi COVID-19 hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.

Mechi zilizofutwa ni za tatu za na za nne kufuzu Fainali za AFCON 2021 ambazo zilipangwa kufanyika kati ya Machi 25 na 31 mwaka huu, kufuzu Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 20 zilizopangwa kufanyika kati ya Machi 20 na 22 na marudiano Machi 27 na 29 mwaka huu.

Aidha, CAF pia imesitisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa (AFCON) kwa Wanawake 2020 zilizopangwa kufanyika kati ya Aprili 8 na 14 mwaka 2020 – na ratiba mpya ya michuano hiyo itatangazwa kwa wakati.

Lakini Ligi Kuu ya Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi moja, Tanzania Prisons wakiwa wenyeji wa Mbao FC kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, huku nyingine sita zikifuata kesho.

CORONA: Serikali ya Tanzania yafunga shule siku 30
Tanzania, Ubelgiji zajadili kuboresha sekta ya kilimo na Madini… Sweden yaahidi ushirikiano