Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemuagiza Katibu Mkuu (Afya) kuwasimamisha kazi, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dkt. Nyambura Moremi na Meneja Udhibiti wa Ubora, Jacob Lusekelo.

Taarifa iliyotolewa leo, Mei 4, 2020 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Idara Kuu Afya, Catherine Sungura imeeleza kuwa Waziri amechukua hatua hiyo baada ya Rais John Magufuli kueleza changamoto ya vipimo vya virusi vya corona katika maabara hiyo.

Aidha, Waziri Ummy ameunda Kamati ya wataalam wabobezi, yenye jumla ya wataalamu 10 kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Maabara hiyo ya Taifa. Kamati hiyo itakayoongozwa na Prof. Eligius Lyamuya pia itakuwa na jukumu la kuufanyia uchunguzi mfumo wa ukusanyaji na upimaji wa sampuli za covid-19.

“Kamati hii inaanza kazi mara moja na inatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya tarehe 13, 2020,” taarifa hiyo imeeleza.

Imeongeza kuwa sambamba na uchunguzi huo, shughuli za upimaji wa sampuli za virusi vya corona katika maabara hiyo zitaendelea.

Akizungumza jana katika tukio la kumuapisha Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Mwigulu Nchemba, Rais Magufuli alibainisha changamoto katika maabara hiyo, ambapo alisema kuwa vipimo vilionesha mbuzi, kware na papai kuwa na virusi vya corona.

Makonda atangaza vita wanaouza sukari bei ghali
CORONA: Paulista ahimiza chanjo kabla ya ligi kuendelea