Neema imeendelea kumshukia mshambuliji na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo, baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya nchini Hispania kwa msimu uliopita, kupitia tuzo za Gazeti La Marca.

Ronaldo ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, ikiwa ni siku moja baada ya kukamilisha mpango wa kusaini mkataba mpya ambao utamuweka Santiago Bernabeu hadi mwaka 2021.

Ronaldo ameshinda tuzo hiyo kufuatia uwezo mkubwa ambao aliuonyesha katika kikosi cha Real Madrid kwa msimu uliopita, jambo ambalo lilitoa msukumo kwa wahusika kumpigia kura nyingi zaidi, tofauti na wapinzani wake.

Ronaldo alifunga mabao 35 na kutoa pasi 11 za mwisho zilizosaidia ushindi kwa klabu yake katika michezo ligi, lakini hatua ya kutwaa ubingwa wa ligi ya Ulaya pamoja na kuiwezesha timu ya taifa lake la Ureno kutwaa kombe la Euro 2016 nayo imeonyesha kuchangia mafanikio anayoendelea kuyapata.

Tuzo aliyotwaa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 inaitwa Alfredo di Stefano, jina la aliyekua mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid.

Hii inakua mara ya nne kwa Ronaldo kutwaa tuzo hiyo, tofauti na kwa mpinzani wake wa karibu Lionel Messi ambaye ameshatangazwa kuwa mshindi mara tano kwa msimu wa 2008/09, 2009/10, 2010/11 na 2014/15.

Tuzo ya kocha bora wa msimu iitwayo Miguel Munoz, ilikwenda kwa meneja wa klabu ya Atletico Madrid Diego Simeone huku  Asier Garitano akichukua tuzo ya kocha bora wa ligi daraja la kwanza.

Alvaro Morata, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji aliyechangia mafanikio ya timu ya taifa.

Sherehe za utoaji wa tuzo hizo zilihudhuriwa na wageni mashuhuri kama rais wa La Liga Javier Tebas, Emilio Butragueno, Fernando Hierro, rais wa Atletico Madrid Enrique Cerezo, pamoja na mtendaji mkuu wa Sevilla CF Jose Castro.

Alexis Sanchez Hatarini Kuikosa Man Utd
Breaking News: Trump amshinda Rasmi Clinton, ndiye Rais Mteule